Somo letu linaendelea. Katika mstari ule
wa Luka 13:22 Biblia inaeleza kuhusu mtu mmoja aliyemuuliza Bwana Yesu
kuhusu wingi wa watu wanaookolewa. Bwana Yesu akijibu swali hilo alisema
kuwa JITAHIDINI KUINGIA KATIKA MLANGO ULIO MWEMBAMBA, KWA MAANA
NAKWAMBIA KUWA WENGI WATATAKA KUINGIA LAKINI WASIWEZE. Pamoja na sababu
nyingi ambazo nimekwisha kuzieleza katika masomo yaliyotangulia, leo
katika Sehemu hii ya Kumi na Nane tunaendelea na sababu nyingine.
23. WATAKOSA MSINGI.
1Kor 3:10-11. “Kwa kadri ya Neema
ya Mungu niliyopewa na Mungu, mimi kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima,
naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake, lakini kila mtu
aangalie anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye
kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani YESU KRISTO.”
Wapendwa, leo tutauangalia Msingi.
Kila nyumba unayoiona ina msingi, na misingi imetofautiana, msingi wa
nyumba ya kawaida ni tofauti na msingi wa ghorofa. Msingi wa ghorofa
Moja ni tofauti na msingi wa ghorofa Kumi. Jinsi ghorofa linavyokwenda
juu ndivyo msingi unatakiwa kwenda chini, na ndivyo inatakiwa pia
wajenzi kuchanganya material kwa kipimo kinachofaa, vinginevyo ghorofa hilo litaishia kuanguka.
Hapo juu tumesoma kuwa hakuna msingi
mwingine nje ya Kristo. Maana yake ni hivi ILE SABABU ILIYOKUFANYA USEME
UMEOKOKA NI MHIMU SANA SANA.
Wengine waliokoka kwa sababu walikuwa
wagonjwa. Walipoambiwa sasa unatakiwa kuokoka, kwa kuwa anaumwa akasema
sawa, si kwamba moyo wake ulimpenda Mungu kwa kweli. Wengine walikutwa
gerezani, walipoambiwa habari ya kuokoka, na wakaambiwa, ukiokoka Mungu
atakutoa jela, na kwa kuwa walikuwa wamebanwa iliwalazimu wakubali na
kweli Mungu aliwafanyia hivyo. Wengine walisikia wahubiri wakisema wewe
unayeteseka na umaskinu njoo kwa Yesu, atakupa kile na kile, na kwa kuwa
walikuwa na hali mbaya wakalazimika kufanya hivyo, na si kwamba mioyo
yao ilikuwa kweli imeamua kumfuata Bwana Yesu.
Utakumbuka siku moja Yesu aliwaambia watu
waliokuwa wanamfuata kuwa, MSIKITENDEE KAZI CHAKULA KINACHOHARIKA,
AKASEMA MNANIFUATA KWA SABABU MLIKULA MIKATE MKASHIBA. Mpendwa hebu
jiulize: KWA NINI UNAMFUATA YESU?
Tuendelee na somo letu katika kuuangalia MSINGI.
Katika Ebr 6:1-6 kuna maneno ambayo nimeyapanga kama ifuatavyo:
“Kwa sababu hiyo tukiacha, kuyanena mafundisho ya kwanza, ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu,
1. TUSIWEKE MSINGI TENA WA KUZITUBIA KAZI ZISIZO NA UHAI.
2. NA WA KUWA NA IMANI KWA MUNGU.
3. NA WA MAFUNDISHO YA MABATIZO.
4. NA KUWEKEA MIKONO.
5. NA KUFUFULIWA WAFU.
6. NA HUKUMU YA MILELE.
Ndugu zangu watoto wa Mungu, Maneno hayo
hapo juu ndiyo misingi ambayo kila aliyeokoka alitakiwa kufundishwa.
Hiyo ndiyo itakufanya uendelee mbele. Hata kama wewe utakuwa ni ghorofa,
hautaweza kuporomoka kamwe!
Sasa tutaendelea kuyapitia moja baada ya
jingine ili uweze kuelewa vizuri. Ni ombi langu kuwa Mungu wetu
aliyetuokoa atatupatia Neema ya kuweza kuelewa vizuri kwa uongozi wa
Roho mtakatifu.
1.Kutubia kazi ambazo hazina uhai.
Ni kitendo cha mtu kutubu dhambi zake kwa mtu. Wengine wanaita
Kuungama. Vyovyote utakavyoiita lakini tunapaswa kuungama dhambi zetu
kwa YESU, na pia ni kuungama na kuziacha, kutozirudia tena.
Mith 28:13 “Afichaye dhambi zake, hatafanikiwa, bali aziungamaye na kuziacha atapata rehema”. Mpendwa Biblia inajieleza. Tunatakiwa tuziungama na kuziacha tofauti na mafudisho mafu kuwa mtu uende kanisani kila jumapili uungame dhambi kwa mtu.
Jumapili hii utaungama kwake, na jumapili ijayo, na ile ijayo, mpaka
mwezi, mpaka mwaka, unaanza tena mwaka mwingine! Hapana. Nenda kwa Yesu,
ungama na kuziacha, utapata rehema.
Katika Yoh 9:31 tunaona
kuwa Mungu hasikii wenye dhambi. Kama utaishi na dhambi, elewa kuwa
Mungu hakusikii kabisa wakati unaomba. Atakusikia pale tu ukiziungama na
kuziacha, tangu hapo atakuwa anakusikia.
Mith 8:13 “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu.”
Unajua wapendwa, kila mtu anasema “kweli namcha Mungu” au “nampenda
Mungu”. Lakini sikia, jipime hapo katika mstari huo unasema kuwa KUMCHA
MUNGU NI KUCHUKIA UOVU.
Hebu tuendelee kuona jinsi ya kuungama au kutubu: Ni kutokurudia yale ambayo mtu ameamua kuyaombea msamaha kwa Mungu. Yaani ni kumaanisha kile unachokisema.
Katika Yoh 5:10-14 kuna kisa cha mtu
aliyekuwa amelala miaka 38, na wengine walikuwa wanaponywa maji
yanapotibuliwa, ila yeye alikuwa haponywi. Siku moja Bwana wa huruma
alimkuta amelala, akamuuliza kama anataka kuwa mzima nay eye akasema
HANA MTU WA KUMTIA KWENYE BIRIKA. Nafikiri hakuwa ameelewa swali. Kama
wengi wetu tusivyoelewa wakati Bwana ansema na sisi. Utakumbuka Adamu
aliulizwa kwa nini UMEKULA TUNDA? AKASEMA NI YULE MWANAMKE ULIYENIPA
NDIYE AMENIPA TUNDA. Kumbe kama angeulizwa kuwa “ni nani amekupa tunda ukala?”
ndipo angejibu hivyo. Pamoja na kutokujibu swali sawa sawa lakini Bwana
akamwambia SIMAMA JITWIKE GODORO LAKO UENDE. Naye akasimama akajitwika
godoro akaenda. Mafarisayo walipomsumbua kuwa mbona amejitwika godoro
wakati ilikuwa ni sabato yeye aliwajibu kuwa yule aliyemfanya awe mzima
ndiye aliyemwambia ajitwike godoro!
Kama vile wengi wetu
tukiishaokoka, watu huwa wanajitokeza kuulizia wokovu wetu, kuwa kwa
nini hili, kwa nini umeacha dini yetu, kwa nini hili na lile. Ebu jibu liwe ni kwamba: “YEYE aliyenifanya mzima ndiye ameniambia nijitwike godoro”
Yoh 5:14 “Baada ya hayo Yesu
akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, angalia umekuwa mzima, usitende
dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi”
Nimesema kutubu au kuungama ni kuacha, ni
kugeuka upande mwingine, ni kuipa dhambi mgongo na kutokuirudia tena.
Unaona Yesu alivyomwambia mtu huyu aliyekuwa amelala miaka 38, kuwa
akirudia litampata baya zaidi ya hilo la kulala miaka 38. Je, ni lipi
hilo baya zaidi?
Biblia inasema pepo akimtoka mtu hurudi
tena, akikuta aliyemfukuza hayumo, huendea wengine SABA walio wabaya
zaidi ya yule, na hali ya mtu huyo huwa mbaya zaidi. Hayo yapo katika Math 12:43
Katika Yoh 8:1-11 tunaona mwanamke mmoja
aliletwa kwa Yesu, alikuwa amekamatwa kwenye zinaa, na wanawake wa namna
ile walikuwa wanapigwa kwa mawe. Siku hiyo aliletwa kwa Yesu, na Yesu
alimhurumia, akawaambia wale washtaki wake kuwa yeyote asiye na dhambi
awe wa kwanza kumtupia jiwe, na wengine wafuate. Yule mwanamke alijua
kuwa amekwisha, pengine alikuwa ameisha wahi kuona wengine wakipigwa kwa
mawe, akawa anasubiri mawe. Biblia inasema Yesu akainama akawa
anaandika chini, hatuelewi alikuwa anaandika nini, lakini wengine husema
alikuwa anaandika dhambi ya kila mtu aliyekuwa pale,
na kila mmoja alipoona vile, alikimbia. Mama yule alibaki peke yake na
Bwana Yesu, na katika Yohana 8:10-11 “ Yesu akajiinua asimwone mtu ila
yule mwanamke, akamwambia mwanamke, wako wapi washitaki wako?
2. Kuwa na Imani kwa Mungu.
Ni kukubaliana na kile ambacho Neno la Mungu linasema, hata kama kwa
macho ya kibinadamu linaonekana kuwa haliwezekani kabisa. Ndiyo maana
mtume Paulo akaandika kuwa: HATUENENDI KWA KUONA, BALI TUNAENENDA KWA
IMANI. Hapo ndipo wanapopatikana au walipopatikana mashujaa wa Imani.
Walikubaliana na Neno la Mungu bila kujali gharama. Wengine
walikubaliana mpaka wakafa bila kubadilisha msimamo wao.
Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo
yatakayokupata, tazama ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani, ili
mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa,
nami nitakupa taji ya uzima.
Yuda 1:5 “Tena napenda
kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kuyajua haya yote, ya kwamba Bwana
akiisha kuwaokoa watu katika Nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale
wasoioamini”
Ndugu yangu, wakati mwingine shetani
analaumiwa bure. Hapo juu unaona kuwa Bwana akiisha kukuokoa unapaswa
kumwamini kuwa anaweza kabisa kukufikisha kule alikokuahidi. Haitakiwi
kumtilia mashaka maana mashaka huletwa na uoga. Uoga ukiishaingia, hofu
inaingia, mashaka naye anasogea, ndipo kutetemeka nako kunakuja kwenye
mwili. Utakumbuka Mungu alimwambia Gidion, katika Waamuzi 7 hivi: “watu
hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika
mikono yao, wasije Israel wakajivuna, juu yangu wakisema, mkono wangu
mwenyewe, ndio ulioniokoa, basi sasa nenda tangaza habari masikioni mwa
watu hawa, na kusema MTU AWAYE YOTE ANAYEOGOPA NA KUTETEMEKA, ARUDI
AONDOKE KATIKA MLIMA GILIADI. NDIPO WATU ISHIRINI NA MBILI ELFU
WAKARUDI, KATIKA WATU HAO, WAKABAKI WATU ELFU KUMI.
Unaona! Mungu haendi na waoga, haendi na
wanaotetemeka, hao ndio unasikia wanakufa na pressure, mishtuko.
Ukiishaokoka hautakiwi kuwa hivyo. Elewa siku zote kuwa VITA SI VYAKO,
ELEWA ALIYEMO NDANI YAKO NI MKUU KULIKO ALIYE KATIKA DUNIA, ELEWA
UNAYAWEZA MAMBO YOTE KATIKA YEYE AKUTIAYE NGUVU.
3. Mafundisho ya Mabatizo.
Mpendwa, ninafundisha Misingi au Msingi wa Mkristo, ambao ukiishakuwa
ndani yako hakuna kitakachokutikisa kamwe. Kumbuka Biblia inasema kuwa
mwenye haki ni jasiri kama SIMBA. Ndiyo maana Bwana wetu Yesu anaitwa
SIMBA WA KABILA YA YUDA. Hata katika Biblia kuna Neno USIOGOPE mara
idadi ya siku za mwaka mzima. Kwa hiyo kila ukiamka asubuhi kuna neno
“USIOGOPE” liko hapo kukusalimia.
Kwa nini Biblia inasema MABATIZO? Haisemi UBATIZO, ni MABATIZO. Hii inaonyesha ni Mengi.
a). Ubatizo wa Maji. Katika Math 3:13
tunamwona Bwana wetu Yesu akienda Yordani kubatizwa. Yohana akambatiza
akiwa mtu mzima tofauti na siku zetu unaona watu wanabatizwa wakiwa
watoto wadogo, na wanatafuta mtu anakuwa baba yake wa ubatizo. Hiyo siyo
Biblia.
Katika Mark 16:14 Biblia inasema AAMINIYE
NA KUBATIZWA ATAOKOKA. Huyo anayebatizwa anatakiwa kuamini yeye
mwenyewe kwa moyo wake, ndipo abatizwe. Kinyume cha hapo tunafundisha
mambo yetu wenyewe, wala siyo ya Mungu.
Rumi 6:4 “Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya UBATIZO”.
Ubatizo ni ishara ya kuwa mtu amekufa, na anazikwa kwenye maji. Wapo
wahubiri wengi wanasema haijalishi ni maji gani, yawe maji mengi au maji
kidogo mradi umebatizwa. Mpendwa, ebu sikia maandiko haya hapa katika
Math 24:4 “Yesu akajibu akawaambia ANGALIENI MTU ASIWADANGANYE”. Ni
juu yangu, ni juu yako, ni juu ya kila mtu kuangalia asidanganywe.
Atakayekubali kudanganywa basi atakapofika kwa Yesu, ataulizwa ilikuwaje
ukafanya hivyo? Atasema nilidanganywa. Nakuambia ndugu yangu kuwa wala
hakutakuwa na msamaha.
Kumbuka Mungu alimuuliza ADAM “Kwa nini umekula tunda nililowakataza kwamba msilile?” Jibu: Mwanamke uliyenipa. ( Bado alipata adhabu}
HAWA naye akaulizwa: “Kwa nini umekula tunda?” Jibu: Nyoka alinidanganya nikala.
Pamoja na majibu hayo mazuri lakini bado hao wazazi wetu wa kwanza
waliadhibiwa tu. Yule aliyepewa na mwanamke, na yule aliyedanganywa,
wote waliadhibiwa!.
Hapo nilikuwa nazungumzia ubatizo wa maji mengi, maana kama Biblia inasema ni ishara ya mazishi, basi tuelewe kuwa mtu akifa huzikwa mwili mzima wala sio kichwa peke yake!
Nadhani utaniuliza swali kuwa, Sasa hao wanaobatiza watoto wadogo, wameyapata wapi hayo mafundisho? JIBU: Mark 7:6-7 “Akawaambia
Isaya alitabiri vema, juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, watu
hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami, nao waniabudu
bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu”. Nakushauri kuwa kila unachofundishwa ebu kikague kama kweli kiko kwenye NENO la Mungu, yaani BIBLIA.
b). Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Mdo 1:6-7 “Basi
walipokutanika, wakamuuliza, wakisema; Je, Bwana wakati huu ndipo
unapowarudishia Israel ufalme? Akawaambia siyo kazi yenu kujua nyakati
wala majira, Baba aliyoweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilkia juu yenu Roho mtakatifu, nanyi
mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalem, na katika Uyahudi wote na
Samaria na hata mwisho wa nchi”
Roho ajapo ndani ya mtu ndiye humpa nguvu za kushinda maovu. Ndiye anakupa nguvu za kuwa shahidi.
Rumi 8:26. Hatujui
kuomba ila Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Roho
wa Mungu alikuwa ndani ya Yesu, ndiye huyo huyo akiwa ndani yako utaishi
kama alivyoishi Yesu. Atakuombea kama alivyomwombea Yesu.
Ebr 5:7 “Yeye
siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa
katika, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa
jinsi alivyokuwa mcha Mungu”. Mpendwa, kama Yesu ndivyo aliishi
duniani, kwa kilio kikuu, naye alisaidiwa na Roho Mtakatifu, basi mimi
na wewe kama tunataka tushinde tunamhitaji Roho mtakatifu, ndiye atakaye
tusaidia.
Gal 4:6 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwetu, aliaye ABA yaani Baba”.
Ndugu yangu pengine umeokoka, au hujaokoka, Ubatizo wa Roho mtakatifu
ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo, na huyo ndiye ataendelea
kukufundisha Neno la Mungu na kukuweka kwenye kweli yote.
c). Ubatizo wa Mateso. Luka 12:49-53. “Nimekuja
kutupa moto duniani, na ukiwa umeishawashwa, ni nini nitakalo zaidi,
lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata
utimizwe. Je, mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani?
Nawaambia la sivyo bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba
moja, watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu wa kwa wawili, wawili
kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, mwana na baba yake, mama na
binti yake na binti na mamaye, mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu”
Hayo yote yanaeleza jinsi safari ya
Mbinguni inavyomkabili mtu peke yake bila kutegemeana. Kwa hiyo
unatakiwa uiangalie Biblia inachokufundisha, kishike, kikumbatie.
Wengine wanasema baba kanizuia kuokoka, mama kanizuia kuokoka, kaka, au
baba mkwe. Hapana! Kila mtu atasimama mbele za Bwana atoe habari zake
mwenyewe.
Bwana akasema anao ubatizo mwingine ambao
ni shida kama nini kuutimiz!. Ndugu zangu, Yesu alikuja akatuachia
kielelezo hapa duniani. Yaliyompata ndio yatatupata. Kama watu
walimpenda, basi watatupenda tu na sisi, kama walimchukia ebu tujue kuwa
yaliyompata ndiyo yatatupata. Ndio maana alisema mtu akitaka kumfuata
AUBEBE MSALABA WAKE AMFUATE. Kumbuka MSALABA maana yake ni MATESO.
Ni kweli kwamba hatuwezi kusulubiwa kama alivyosulubiwa, ila tunasulubiwa kwa namna moja au nyingine.
Mdo 14:21-22. “Hata walipokwisha
kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea
mpaka Listra, na Ikonio, na Antiokia (yafuatayo nimeyapanga mwenyewe
kuwa):
i. WAKIFANYA IMARA ROHO ZA WANAFUNZI.
ii. WAKIWAONYA WAKAE KATIKA ILE IMANI.
iii.WAKIWATAARIFU KUWA TUMEPASWA KUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU KWA NJIA YA DHIKI NYINGI.
Ndugu zangu wapendwa, kusudi la Injili ya Kristo tunayoihubiri linatakiwa kuwa katika sehemu hizo 3.
Kufanya roho za wanafunzi kuwa imara.
Kwa nini zifanywe Imara? Kwa kuwa baada ya kuokoka huwa tunakutana na
mambo mazito kiasi kwamba kama mioyo yetu haiko imara kwa Neno la Mungu,
hatuwezi kufika popote. Tutaishia kusema tu nimeokoka, lakini mwisho wa
siku, unakuta moyo huo ambao haukufanywa imara umebomoka. Ndio maana
kwenye milango yetu tunaweka makomeo, na tukiisha funga twaweza kulala.
Na mioyo yetu inatakiwa kufanywa Imara. Ndiyo maana imeandikwa katika
Mith 4:23 kuwa “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, maana huko ndiko
zitokazo chemi chemi za uzima”. Na moyo unalindwa kwa NENO la Mungu.
Ndiyo maana imeandikwa kuwa NENO LA KRISTO LIKAE KWA WINGI NDANI YETU.
Kazi ya 3: Kuwataarifu kuwa kuingia
mbinguni ni kwa njia ya dhiki nyingi. Ndugu yangu, Biblia vile
ilivyoandikwa ndivyo ilivyo. Hatupaswi kuigeuza, wala kuichakachua, au
kuigoshi, imeeleza wazi wazi kuwa tutaingia kwa njia ya DHIKI NYINGI.
Pata muda soma vizuri Neno katika kitabu cha MASHUJAA WA IMANI, cha
Waebrania sura ile ya 11.
1Pt 2:18-23. “Enyi watumishi,
watiini bwana zenu, kwa hofu nyingi, sio wao walio wema na wapole tu,
bali nao walio wakali, maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni
kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki, kwa maana ni sifa gani
kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi. Lakini kustahimili
mtendapo MEMA NA KUPATA MATESO, huu ndio wema hasa mbele za Mungu, maana
ndiyo mlioitiwa, maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia
kielelezo mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila
haikuonekana kinywani mwake, yeye alipotukanwa hakurudisha matukano,
alipoteswa, hakuogofya, bali alijikabidhi kwake ahukumuye kwa haki”.
Ndugu yangu, ebu soma
hayo maandiko hapo juu. Mimi na wewe tujipime kwake huyo ambaye
tunaambiwa tufuate nyayo zake. Je, tunazikanyaga nyayo zake kweli? Au
zetu zimepanuka? Au zimepwaya?
2Timotheo 3:10-12. “Bali wewe
umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, makusudi yangu, na Imani
na uvumilivu, na upendo na saburi, tena na adha zangu na mateso, mambo
yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonia, na katika Listra, kila
namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.
Naam na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa wataudhiwa.”
Mistari hiyo inatuonyesha jinsi watumishi
wa kweli walivyoishi, ambao Biblia inasema wazi wazi kuwa TUMEJENGWA
KATIKA MSINGI WA MITUME NA MANABII. Kwa kusema hivyo ni kwamba njia
waliyoipitia ndiyo tutaipitia, ambayo ndiyo ile Bwana wetu Yesu
aliipitia. Ndio maana walikuwa wakipita na kuwajulisha kuwa wakae
wakijua kuwa TUTAINGIA KWA NJIA YA DHIKI NYINGI.
Ndugu zangu leo nitaishia hapa katika sehemu hii ya Kumi na Nane. Misingi mingine iliyobakia, ambayo ni Kuwekea Mikono, Kufufuliwa Wafu na Hukumu ya Milele nitaielezea katika Sehemu ifuatayo ya Kumi na Tisa.
Ndugu mpendwa, ninakushauri kuwa baada ya
kusoma Misingi hiyo niliyoielezea jikite katika kuitafakari na
kuitendea kazi ili roho yako ipate kuwa imara katika safari hii, kwa
maana ya kwamba dhiki zitakapokuja wala usishangae, na uwe na uwezo wa
kupita na upate kuitwa MSHINDI!
Ubarikiwe na Bwana.
Ndugu yenu Mchungaji Samuel Imori.